Kituo cha Televisheni cha Azam kimeingia makubaliano ya mwaka mmoja ya kuonesha mubashara mashindano ya Ndondo hatua ya makundi Mkoa wa Da...

Akizungumza baada ya kutia saini makubaliano hayo jana, Mkurugenzi wa Azam TV, Tido Muhando alisema wameingia makubaliano na Clouds Media ili kuwaonesha watu wasioweza kufika katika viwanja kushuhudia mashindano hayo.
“Tunawaahidi Clouds Media na Watanzania tutafanya kazi nzuri kwani sisi ndio kituo bora kwa urushaji wa matangazo hasa soka hilo halina ubishi,” alisema Tido. Naye Mratibu wa Ndondo Cup, Shafii Dauda aliwashukuru Azam Media kuwa sehemu yao katika kuendesha mashindano hayo kwa miaka minne mfufulizo.
“Lengo la mashindano ni kutengeneza daraja kwa vijana wenye vipaji ili waonekana na wasajiliwe na timu za madaraja ya juu hivyo tunaishukuru Azam Media kuwa sehemu yetu kufanikisha ndoto za vijana,” alisema Shafii.
Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam, Almas Kasongo aliishukuru Azam Media na Clouds Media kwa kusaidia kuendeleza michezo Dar es Salaam. “Tunafurahi kuona soka likichezwa katika mkoa wetu kwani mnasaidia kutekeleza moja ya majukumu yetu hivyo nawaahidi mashindano haya yatasimamiwa kwa weledi mkubwa,” alisema Kasongo.
Droo ya makundi ya mashindano hayo inatarajiwa kuchezeshwa leo katika viwanja vya Escape One, Kinondoni ambapo timu 32 zitakuwa kwenye bakuli moja. Timu hizo ni Vituka FC, Twiga International, Kigoma Kombaini, Stimtosha, Tandavamba, Black Six, Ukwamani, Ndanda Investment, Miami, Mpakani Kombaini na Kibo Kombaini.
Vijana rangers, Goroka FC, Burudani, Polisi DSM College, Faru jeuri, Boom FC, Temeke Market, Temeke Squad, Tabata United, Misosi, Keko Furniture na Buguruni United. Nyingine ni Goms United, Kigogo Kombaini, Wauza matairi, Shelaton, Makuburi, Kibada One, Kauzu FC, Mlalakuwa Rangers na Madiba FC.